Wabunge wa chama cha Jubilee inadaiwa kuwa wako katika harakati kufanya hivyo wakati Chama cha Mahakimu na Majaji (KMJA) kimesema hilo linatokana na Mahakama ya Juu kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa urais wa Agosti 8.
Gazeti la the Nation limejiridhisha kuwa mpango huo wa wabunge kufungua madai ndani ya Bunge dhidi ya Jaji Maraga na Amadi litafanyika wakati watapokuwa wamemaliza mafunzo na kupata uzoefu na shughuli za bunge.
Njama hiyo ni kumhujumu Jaji Mkuu na Msajili bila ya kuwepo tuhuma zozote na baada ya hapo kupitisha azimio katika Bunge kuwa wachunguzwe na Tume ya Maadili na Kupambana na Rushwa (EACC), chanzo katika bunge kimesema.
Lakini hilo linafanyika siyo kwa sababu tuhuma hizo ni nzito lakini kwa ajili ya kuwadhalilisha,” chanzo chenye uzoefu na hujuma hizi kimesema.
Chanzo hicho, ambacho ni Mbunge, pia kimeeleza kuwa Taasisi ya EACC itatumika kama “upanga” kwa sababu wale walioandaa hujuma hiyo wanajua wazi kuwa hawawezi kumuondosha Jaji Mkuu na Msajili kupitia Tume ya Huduma za Mahakama.
“Hivi sasa watu hao wanataka kumpaka matope Jaji Mkuu kwa tuhuma za uongo,” chanzo hicho kimesema.
Katibu Mkuu wa KMJA Bryan Khaemba amesema kuwa watafanya kila wanaloweza kutetea uhuru wa Mahakama.
“Tunafahamu kuwa kuna hujuma hiyo inayoandaliwa na baadhi ya wabunge kutaka kuwaondoa kwa nguvu Mheshimiwa Jaji Mkuu na Msajili wa Mahakama katika nafasi zao, baada ya kubatilisha uchaguzi wa rais hivi karibuni.
Napenda kuwakumbusha wanaotaka kufanya hujuma kwamba maana halisi ya utawala wa sheria, ni kuwa nchi inaongozwa na sheria na sio watu,” Khaemba amesema.
Hatua hii imejitokeza kipindi kifupi baada ya Mbunge wa mji wa Nyeri Mr Ngunjiri Wambugu kufungua madai mbele ya Tume ya Huduma za Mahakama akitaka Jaji Maraga avuliwe madaraka.
Jaji Maraga ni mwenyekiti wa Tume ya Huduma za Mahakama na Amadi ni katibu wa tume hiyo.
Khaemba amesema kuwa kutokubaliana na uamuzi wa mahakama ni sawa katika mifumo ya kisheria lakini ni lazima lifanyike kwa kuzingatia Katiba.
"Tunachokiona hapa ni jaribio la watu wachache ambao wanataka kudai kuwa wako juu ya Katiba. Pale tu unapoanza kudadisi uhuru wa mahakama, tayari unakuwa umekiuka kifungu cha pili cha Katiba," amesema.