Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito wa msaada mkubwa wa kimataifa kwa Somalia wakati wa ziara yake katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki ambayo inakabiliwa na ukame mbaya kuwahi kushuhudiwa katika miongo kadhaa.
Guterres alisema Somalia inakabiliwa na matatizo ya kibinadamu na wakati huo huo inapambana na tishio kubwa la ugaidi. Guterres akiwa katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari na Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia aliwaambia waandishi wa habari kwamba nipo hapa kupaza sauti juu ya haja ya uungwaji mkono mkubwa wa kimataifa kwa sababu ya matatizo ya kibinadamu ambayo nchi inashuhudia.
Katibu mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa alipokelewa kwa hadhi ya kutandikiwa zulia jekundu na heshima ya kupita kwenye kikosi cha walinzi alipopokelewa katika uwanja mkuu wa ndege wa kimataifa na maafisa wa Somalia pamoja na Umoja wa Mataifa.
Alimshukuru Rais Mohamud kwa mapokezi hayo mazuri na akasema anatarajia kujumuika nao kwenye futari ya mfungo wa Ramadhan baadaye leo Jumanne.