Iwapo kura hiyo ya maoni itaidhinisha katiba mpya, itaweka ukomo wa mihula miwili ya urais, kuondoa nafasi ya waziri mkuu na kutambua Kifaransa kama lugha rasmi ya Gabon. Vilevile, muda wa kuhudumu kama rais utaongezwa na kuwa miaka saba.
Jenerali Brice Oligui Nguema, rais wa mpito aliyenyakua madaraka katika mapinduzi mwaka jana, anawataka wapiga kura kupitisha katiba mpya, ambayo anasema inadhihirisha dhamira ya serikali ya nchi hiyo katika kuandaa mkondo mpya wa Gabon.
Maafisa wa kijeshi waliipindua serikali mwezi Agosti mwaka jana. Rais aliyepinduliwa, Ali Bongo, alitawala tangu 2009. Baba yake, Omar, alikuwas ametawala tangu 1967.
Yalikuwa ni mapinduzi ya nane katika Afrika Magharibi na Kati tangu mwaka 2020. Mataifa yenye nguvu ya Magharibi na vyombo vya kanda yamewashinikiza watawala wa kijeshi kufanya uchaguzi ndani ya muda muafaka.