Chama cha African National Congress (ANC) kilisema Ramaphosa, ambaye ataongoza kile inachokiita serikali ya umoja wa kitaifa (GNU), atatangaza “baraza la mawaziri shirikishi GNU” baada ya uchaguzi mkuu wa Mei 29 kutotoa mshindi wa moja kwa moja.
Salamu za pongezi ziliendelea kumiminika kwa kiongozi huyo ambaye alichaguliwa tena kuwa rais siku ya Ijumaa na ataapishwa Juni 19.
Uchaguzi huo uliashiria mabadiliko ya kihistoria kwa Afrika Kusini, na kumaliza miongo mitatu ya utawala wa ANC wa hayati Nelson Mandela.
Wakati huo huo rais wa Marekani Joe Biden leo Jumamosi alimpongeza mwenzake wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, kwa kuchaguliwa tena, baada ya chama cha African National Congress kuunda serikali ya mseto ambayo haijawahi kutokea.
"Ninatarajia Marekani na Afrika Kusini kuendelea na kazi yetu pamoja, kupanua fursa za kiuchumi, kuwekeza katika ufumbuzi wa nishati safi, na kuonyesha kwamba demokrasia inaleta matokeo," Biden alisema katika taarifa yake.